RUGBY: Shujaa yashika namba mbili huku Lionesses ikishika mkia
2021-02-23 15:36:24| cri

Kenya imekamilisha mashindano ya kwanza ya raga ya wachezaji saba kila upande ya Madrid Sevens nchini Uhispania, Jumapili, kwa timu ya wanaume kushika nafasi ya pili na ya wanawake nafasi ya sita ambayo ni ya mwisho. Shujaa ilipoteza 21-14 mikononi mwa Argentina katika fainali ya wanaume ya duru hiyo iliyofanyika Februari 20-21, huku Lionesses ikichabangwa 12-10 na wenyeji Uhispania katika mechi ya kuamua nani kati ya wawili hao anavuta mkia. Timu tano zilishiriki kitengo cha wanaume baada ya Ufaransa kujiondoa, na sita ziliwania ubingwa wa kinadada ikiwemo Ufaransa. Duru ya pili itaandaliwa Februari 27-28 mjini Madrid, ambayo itajumuisha duru mbili baadaye mwezi ujao nchini Milki za Falme za Kiarabu na mbili nchini Ufaransa mwezi Mei, ikiwa ni maandalizi ya timu kwa michezo ya Olimpiki ama mechi za kufuzu kushiriki Olimpiki. Shujaa na Lionesses zilifuzu kushiriki Olimpiki jijini Tokyo mwaka 2019.