Kenya: MKU, WEF Waingia Katika Mkataba Wa Kuinua Wanawake Kiuchumi
2021-02-23 15:32:09| cri

CHUO Kikuu cha Mount Kenya (MKU) kimeingia katika mkataba wa maelewano na kikundi cha wanawake cha Women Enterprise Fund (WEF) kwa lengo la kuwapa mwongozo wa kibiashara.

Kikundi hicho kipo chini ya Wizara ya Masuala ya Umma, Vijana na Maswala ya Jinsia.

Kikundi hicho kilibuniwa mwaka wa 2007 kwa lengo la kuwahamasisha wanawake jinsi wanavyoweza kupanua biashara zao na kujitegemea wenyewe.

Mkurugenzi wa maswala ya ushirikiano wa kimaendeleo MKU Prof Peter Wanderi, alisema ushirikiano wao na kikundi hicho ni hatua ya kupongezwa na wengi kwa sababu utaimarisha ujuzi wa kibiashara kwa kujitegemea.

Kikundi hicho tayari kimefadhiliwa kikamilifu na serikali huku wakihimizwa kuzingatia maswala ya kibiashara.

Kwa Sh5 bilioni walizokuwa wamehifadhi kikundi hicho kimepanua uwekezaji na kuweka fedha zao na kufikia Sh20 bilioni.

Ushirikiano huo utafanya juhudi kuona ya kwamba kikundi hicho kinapewa mafunzo kamili ya kibiashara na baadaye kupewa vyeti vyao vya kufuzu baada ya kukamilisha masomo yao.

Kikundi hicho cha Women Enterprise Fund (WEF), kimeweza kusambaza takribani Sh20.4 bilioni kwa vikundi 116,531 vya kujitegemea.

Baadaye wanawake wapatao 1.8 milioni wamenufaika huku asilimia 97 wakilipa mikopo yao bila kuchelewa.

Kulingana na mipango yao wanawake wapatao 1.4 milioni wamepokea mafunzo rasmi ya kibiashara huku idadi ya wanawake 21,000 wakipewa mwongozo wa kupata soko la biashara na kuunganishwa na biashara kubwa sehemu tofauti za nchi.

Kati ya mwaka wa 2019 hadi 2024 kikundi hicho kimeweka mikakati ya kuona ya kwamba wanatafuta soko la biashara na mashirika mengine kwa lengo la kupiga hatua zaidi na kuongeza maarifa katika kazi zao.