Viongozi wawili wa majimbo ya Somalia wapewa mwito wa kushiriki kwenye mazungumzo ya kuondoa mkwamo wa uchaguzi
2021-02-23 09:00:04| CRI

Rais Mohamed Farmajo wa Somalia amewataka viongozi wawili wa majimbo ya Somalia kushiriki kwenye mazungumzo ya majadiliano yenye lengo la kuondoa mkwamo unaochelewesha uchaguzi wa nchi hiyo.

Rais Farmajo amesema viongozi wa Jubbaland na Puntland wanatakiwa kushiriki kwenye mazungumzo yanayopangwa kufanyika kwa mujibu wa mapendekezo yaliyotolewa wiki iliyopita na kamati ya ufundi iliyoteuliwa na serikali kuu na majimbo, kuhusu mkwamo wa uchaguzi.

Rais Farmajo alitoa mapendekezo hayo baada ya kufanya mazungumzo na wakuu wa majimbo mengine na gavana wa eneo la Benadir.

Hata hivyo Rais wa Jubbaland Bw. Ahmed Madobe na Rais wa Puntland Bw. Saidi Abdullahi wamesema hawawezi kushiriki kwenye mazungumzo hayo hadi masharti yao yatakapotimizwa. Moja ya sharti lao ni Rais Farmajo kutoshiriki kwenye mazungumzo hayo kwa kuwa muda wake wa urais uliisha Februari 8.