BASKETBALL: Kenya Morans yafuzu kushiriki AfroBasket 2021
2021-02-23 15:37:05| cri

Timu ya mpira wa vikapu ya wanaume ya Kenya almaarufu Morans, itarejea nchini Kenya usiku wa leo kutoka Cameroon ilikoandikisha historia kwa kuifunga miamba Angola na kufuzu kushiriki Kombe la Afrika (AfroBasket) 2021. Morans, ambayo inanolewa na raia wa Australia Elizabeth Mills, imeingia katika AfroBasket kwa mara ya kwanza tangu mwaka 1993. Wakenya walimaliza Kundi B katika nafasi ya tatu kwa alama nane. Walipata tiketi baada ya kuwafunga mabingwa mara 11 Angola kwa vikapu 74-73 wiki iliyopita.