Balozi wa Italia nchini DRC auawa kwenye barabara iliyotajwa kuwa salama
2021-02-23 08:59:39| CRI

Msemaji wa Umoja wa mataifa Bw. Stephane Dujarric amesema balozi wa Italia nchini DRC Bw. Luca Attanasio ameshambuliwa na kuuawa kwenye barabara moja iliyotajwa kuwa salama, akiwa njiani kuelekea kwenye shule moja iliyo chini ya Shirika la Mpango wa Chakula la Umoja wa Mataifa WFP mjini Rutshuru.

Bw. Dujarric amesema balozi huyo alikuwa akitokea mjini Goma, na ameuawa pamoja na watu wengine wawili aliokuwa akisafiri nao, mmoja akiwa ni mwanausalama wa Italia, na mwingine ni dereva mwenyeji wa WFP. Bw. Dujarric pia amesema kuna makundi kadhaa ya waasi katika eneo hilo, lakini hakutaka kutoa shutuma zozote.

Naibu katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa anayeshughulikia operesheni za ulinzi wa amani Bw. Jean Pierre Lacroix amesema msafara wa magari mawili ya WFP ulishambuliwa katika barabara iliyotajwa kuwa ni salama.