Wafugaji kuku Tanzania watakiwa kukumbatia ufugaji wa kisasa
2021-02-26 16:38:12| cri

Kaimu mkurugenzi wa Kituo cha Utafiti wa Mifugo Tanzania TALIRI Aluna Chawala, amewataka wafugaji wa kuku kuzingatia ushauri unaotolewa na watafiti wa mifugo kwa kukumbatia ufugaji wa kisasa na kuinuka kiuchumi.

Chawala ametoa ushauri huo ikiwa ni siku chache baada ya Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi wa Tanzania kukutana na wafugaji kuku na kubainisha mifugo hiyo sasa itauzwa kwa kupimwa katika mizani badala ya kukadiria.

Alisema hivi sasa wafugaji wanapaswa kufuga kisasa kutokana na mifugo hiyo kuanza kuuzwa kwa kupima kwa kilo katika mizani badala ya kukadiria, uamuzi ambao anaamini utasaidia kupata faida.

Pia, alisema kuku anapofugwa kisasa kwa kupata matunzo mazuri kutoka kwa mfugaji, lazima atakuwa na uzito mkubwa ambao utasaidia kuuzwa kwa bei nzuri sokoni. Aliwataka wafugaji kuzingatia elimu ya ufugaji kuku kisasa inayotolewa na watafiti mbalimbali, ili kuhakikisha wanafuga kisasa na kupata kipato kikubwa ambacho kitawasaidia wao na familia zao.