PARALYMPICS: Tanzania kusaka tiketi ya kufuzu Paralimpiki
2021-03-02 16:33:55| cri

Tanzania inatarajia kushiriki Mashindano ya Dunia kwa ajili ya kufuzu kwa michezo ya Paralimpiki itakayofanyika katika nchi tofauti tofauti. Michezo ya Paralimpiki imepangwa kuanza kutimua vumbi Agosti 24 hadi Septemba 5, mwaka huu mji wa Tokyo, Japan. Katibu Mkuu wa Kamati ya Paralimpiki Tanzania (TPC), Ramadhan Namkoveka, amesema michezo ambayo kamati imeipa kipaumbele ni riadha, mchezo wa kunyanyua vitu vizito na kuogelea kwa watu wenye Ulemavu. Amesema mashindano hayo yanafahamika kama Tunis 2021 World Para Athletics Grand Prix – TUNISIA – yatakayofanyika kuanzia Machi 14 hadi 21 mwaka huu nchini humo, mchezo wa kunyanyua vitu vizito umepangwa kufanyika Juni 16 hadi 21, mwaka huu katika nchi za Colombia, Thailand, Uingereza, Gerogia na Falme za Kiarabu katika Jiji la Dubai, huku mchezo wa kuogelea umepangwa kufanyika Aprili 8 hadi 11, mwaka huu, Sheffield, Uingereza, na pia Aprili 15 hadi 17 mwaka huu, Lewisville, na Dallas Taxes nchini Marekani.