Huduma ya kuandikisha ndoa kwa kujihudumia mwenyewe yazusha mjadala
2021-03-03 15:34:59| cri

Baadhi ya miji katika mkoa wa Jiangsu, mashariki mwa China wamekuwa na mjadala kwenye mitandao ya kijamii Alhamisi, baada ya kuzindua mashine za kuandikisha ndoa kwa kujihudumia, hatua ambayo inaweza kupunguza muda wa kuandikisha ndoa kutoka dakika 15 hadi 20 hadi kufikia dakika tano. Wanamtandao wameeleza wasiwasi wao kuwa huduma hiyo inaweza kudhoofisha hisia za thamani na urasmi wa ndoa.

Ili kupata cheti cha ndoa,wanandoa wapya wanahitaji tu kuscan hati zao za utambulisho, ikiwemo kadi ya kitambulisho na cheti cha ukazi, na halafu wanatakiwa kuingiza taarifa binafsi kwenye mfumo wa mtandaoni. Mfanyakazi mmoja wa Kituo cha usajili wa ndoa cha Xinghua mjini Taizhou amesema, “itakuwa rahisi kama kukata tiketi ya treni.”

Wanamtandao wengi wa China wamelalamika kuwa mchakato huu rahisi wa kusajili ndoa unaharibu hisia za thamani na urasmi wa kufunga ndoa, ambayo huwa ni jambo kubwa katika maisha ya kila mtu. Wengi wamesema bado wanapendelea njia ya zamani inayohusisha huduma za ofisa wa usajili.

Baadhi wanaona mashine hizo zinaweza kusababisha ndoa zisizo za makini, na kuwafanya vijana waone kuwa kufunga ndoa ni jambo rahisi na dogo tu.

Wengine wameeleza wasiwasi kuwa hatua hiyo pia inaweza kuleta matatizo ya kisheria, kwa kuwa watu wenye tatizo la akili wanaweza kudanganywa kuscan hati zao za utambulisho na kufunga ndoa bila hiari au kibali chao cha kweli.