China yasisitiza kuwa mafanikio ya uvumbuzi yanapaswa kunufaisha dunia nzima
2021-03-04 14:51:36| CRI

 

 

Ripoti iliyotolewa hivi karibuni na Shirika la Hakimiliki za Ubunifu Duniani inaonesha kuwa, China imeshika nafasi ya kwanza duniani kwa idadi ya maombi ya hataza za kimataifa kwa miaka miwili mfululizo. Msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya China Bw. Wang Wenbin, amesema jambo hilo linaonesha uwezo mkubwa wa uvumbuzi na ongezeko la mwamko kuhusu hakimiliki za ubunifu nchini China.

Bw. Wang amesema ongezeko la maombi ya China ya hataza za kimataifa linaonesha mafanikio ya China katika kulinda hakimiliki za ubunifu, na pia linamaanisha kwamba China inageuka kuwa nchi yenye uwezo mkubwa wa uvumbuzi kutoka nchi inayoingiza uvumbuzi.

Aidha amesisitiza kuwa, mafanikio ya uvumbuzi yanapaswa kunufaisha dunia nzima, na China inapenda kushirikiana na nchi mbalimbali duniani, kuimarisha ushirikiano katika uvumbuzi wa teknolojia, na kutoa mchango zaidi kwa maendeleo endelevu, shirikishi na yenye uwiano ya hakimiliki za ubunifu duniani.