Ethiopia yatoa tahadhari ya kuongezeka kwa kasi kwa maambukizi ya COVID-19
2021-03-05 18:09:05| cri

Wizara ya Afya nchini Ethiopia imetoa tahadhari kuwa, maambukizi ya virusi vya Corona yanaendelea kuongezeka kwa kasi nchini humo kutokana na watu kutochukua hatua za kujikinga.

Akizungumza na vyombo vya habari vya nchini humo jana jioni, waziri wa wizara hiyo Lia Tadesse amesema, kuna kesi mpya 8,000 za virusi vya Corona na watu 123 zaidi wamefariki kutokana na virusi hivyo.

Amewataka Waethiopia kuendelea kuwa makini dhidi ya kuenea kwa virusi hivyo, akisema kuwa kiwango cha maambukizi ya virusi vya Corona kimeongezeka kutoka asilimia 10 mpaka 13 katika wiki za karibuni.

Mpaka kufikia jana Alhamis jioni, Ethiopia ilirekodi kesi 162,954 zilizothibitishwa kuwa na virusi vya Corona, huku idadi ya watu waliofariki ikifikia 2,394.