Zanzibar yawakaribisha wawekezaji wa Indonesia
2021-03-05 18:57:44| cri

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi amewakaribisha wawekezaji kutoka Indonesia kuwekeza Zanzibar kutokana na kuwepo kwa mazingira mazuri yaliyowekwa na Serikali yake.

Rais Dk. Mwinyi aliyasema hayo baada ya kufanya mazungumzo na Balozi wa Indonesia nchini, Prof. Ratlan Pardede.

Dk. Mwinyi alisema Serikali imedhamiria kuimarisha uchumi wake, hivyo iko tayari kushirikiana na washirika wengine wa maendeleo ikiwamo Indonesia.

Alisema Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Zanzibar zina uhusiano na ushirikiano wa muda mrefu na Indonesia hasa katika uimarishaji wa sekta mbalimbali za maendelo.  Ameongeza milango iko  wazi kwa wawekezaji wa Indonesia kuja kuwekeza Zanzibar.

Alisema Zanzibar ina maeneo kadhaa ya kushirikiana na Indonesia hasa ikizingatiwa kwamba nchi hiyo imepiga hatua kubwa kiuchumi.

Alisema Zanzibar iko tayari kuwakaribisha wawekezaji kutoka Indonesia kuja kuwekeza katika sekta ya bandari. Aidha Mwinyi alimueleza Balozi huyo kwamba sekta ya utalii ina fursa nyingi za uwekezaji. Alieleza Zanzibar imejaaliwa kuwa na vivutio kadhaa vya utalii, hivyo milango yake iko wazi kwa wawekezaji wa sekta hiyo kutoka Indonesia.  

Kwa upande wake, balozi Pardede alisema Serikali yake itaendelea kuiunga mkono Zanzibar katika kuimarisha uchumi wake ikiwamo kuitangaza zaidi Zanzibar kwa wawekezaji wa Indonesia.