UNEP yasema lengo la kumaliza njaa linaweza lisitimie kutokana na uharibifu mkubwa wa chakula
2021-03-05 19:13:13| cri

Shirika la Mazingira la Umoja wa Mataifa (UNEP) limesema, lengo la kuondoa uhaba wa chakula na utapiamlo duniani liko hatarini kwa kuwa asilimia 17 ya chakula kinaharibiwa na walaji.

Hayo yamo kwenye Ripoti ya Uharibifu wa Chakula iliyoandaliwa na UNEP pamoja na shirika la hisani la WRAP la Uingereza iliyotolewa jijini Nairobi, Kenya, hapo jana.

Mkurugenzi mkuu wa UNEP Inger Andersen amesema, kupunguza uharibifu wa chakula kutapunguza utoaji wa hewa chafu, kupunguza uharibifu wa mazingira kupitia uharibifu wa ardhi na uchafuzi wa hewa, kuongeza upatikanaji wa chakula, na hivyo kupunguza njaa na kuokoa fedha.

Amesema serikali, viwanda na wananchi wanatakiwa kushirikiana kwa pamoja kupunguza uharibifu wa chakula na kuimarisha hatua za kudhibiti athari za mabadiliko ya tabianchi, kupunguza upotevu wa anuai ya baiolojia, na uchafuzi wa hewa.