Ndoa kati ya mzee wa miaka 55 na msichana wa miaka 20 mwenye tatizo la kiakili yazindua mjadala kwenye jamii
2021-03-09 11:34:52| cri

Video inayoonesha mzee mwenye umri wa miaka 55 akimwoa msichana wa miaka 20 mwenye tatizo la kiakili mkoani Henan imezusha mjadala mkubwa kwenye mitandao ya kijamii nchini China, na wanamtandao wengi wameeleza mashaka juu ya madhumuni ya familia hizo mbili nyuma ya ndoa hiyo.

Katika video hiyo iliyotangazwa kwenye mtandao wa kijamii wa Weibo, bibi harusi huyo anaonekana bado mdogo sana na analia machozi huku bwana harusi akiwa karibu naye kumfuta pua kwa kutumia tishu. Habari zinasema watu hao walifanya harusi lakini hawajajiandikisha rasmi kupata cheti cha ndoa. Wanamtandao wengi wameeleza mashaka juu ya madhumuni ya familia hizo mbili nyuma ya ndoa hiyo isiyo ya kawaida, na kuuliza kama ndoa hiyo ni halali au la.

Kwa mujibu wa sheria za China, hao wawili kuishi pamoja hakukiuki sheria, lakini hawawezi kupata cheti cha ndoa, kwa sababu tatizo la akili la msichana huyo linamaanisha kuwa hawezi kueleza bayana nia yake ya kuolewa. Lakini kutokana na sera husika, kama hawa wawili wakipata watoto katika siku zijazo, wanaweza kuomba kibali cha uzazi (birth permit) na kuandikisha kwa ajili ya cheti cha ukazi (household registration).

Hata hivyo, bwana harusi huyo amesema ndoa hiyo imekubaliwa na mama wa msichana huyo na kuahidi kwamba atakuwa mume mzuri.