Mbunge wa China apendekeza kuiondoa lugha ya Kiingereza kwenye mtaala wa elimu ya lazima
2021-03-09 11:29:24| cri

Kwenye Mikutano Miwili iliyofanyika mwaka huu hapa Beijing, mbunge mmoja amewasilisha pendekezo la kuiondoa lugha ya kiingereza kama moja ya masomo makuu kwenye mtaala wa elimu ya lazima, na kuzusha mjadala mkubwa kwenye mitandao ya kijamii nchini China.

Baadhi ya wataalam wanaona pendekezo hilo linaonesha wazo la maoni ya mkumbo Populism na lina uwezekano mdogo wa kukubaliwa. Nafasi muhimu ya China kwenye utandawazi duniani inamaanisha kuwa China inahitaji lugha ya kimataifa kubadilishana maoni na teknolojia na nchi za nje. Lakini baadhi wanaona pendekezo hilo linafaa kwa sababu wachina wengi hawatumii lugha ya kiingereza katika maisha yao, licha ya kwenye kipindi cha elimu tu.

Mbunge aliyewasilisha pendekezo hilo anaona muda wanaotumia wanafunzi kujifunza lugha ya Kiingereza hautaleta matokeo linganishi kwenye ajira zao katika siku zijazo, na masomo ya Kiingereza yanachukua asilimia 10 ya jumla ya muda wa masomo darasani, lakini lugha hiyo inatumiwa na chini ya asilimia 10 ya wahitimu wa vyuo vikuu.

Mbunge huyo anaona teknolojia ya Akili Bandia, kama vile vifaa vya kutafsiri, inaweza kuondoa kizuizi cha lugha katika siku zijazo, badala ya mafunzo ya lugha ya Kiingereza kwenye elimu ya lazima.

Mbunge huyo amependekeza wanafunzi wa China kutumia muda mwingi zaidi katika masomo mengine kama vile muziki, michezo na sanaa, na kuweka mkazo zaidi katika kukuza uwezo wao wa kufanya uvumbuzi.

Kura za maoni zilizofanyika mtandaoni zinaonesha kuwa wengi zaidi wanaunga mkono kuendelea kubakiza somo la Kiiingereza kwenye mtaala wa elimu ya lazima, kwa kuwa wanaamini lugha hiyo ni muhimu kwa wanafunzi kushiriki kwenye ushindani wa kimataifa. Wengine pia wameeleza kuunga mkono pendekezo hilo wakisema wanapendelea kutumia muda wa kujifunza lugha hiyo kujifunza Kichina na utamaduni.