Wanafunzi wanaosoma katika vyuo vikuu vya nje walazimika kuhudhuria masomo ya mtandaoni usiku wa manane kutokana na tofauti za wakati
2021-03-22 14:32:29| cri

Katika mwaka mmoja tangu janga la virusi vya Corona lilipuke, athari zake bado zinaendelea katika dunia nzima mpaka leo. Janga hilo limevuruga maisha ya watu wengi, wakiwemo wanafunzi wanaosoma katika vyuo vikuu vya nje.

Hivi sasa wakati vyuo vikuu vingi vya China vimefunguliwa tena, baadhi ya nchi zinazopokea wanafunzi wengi wa kimataifa bado zinatekeleza hatua za zuio, na kuvilazmisha vyuo vikuu vingi vya nje kufundisha kwa kutumia mtandao, hali ambayo imewalazimisha wanafunzi wa China wanaosoma katika vyuo vikuu vya nje kuamka usiku wa manane ili kuhudhuria masomo ya mtandaoni kutokana na tofauti za wakati.

Mbali na hayo, sehemu nyingine muhimu ya uzoefu wa kusoma katika nchi nyingine ni kujionea mwenyewe maisha na utamaduni wa kigeni. Lakini kutokana na janga hilo, wanafunzi wamelazimika kukaa nyumbani tu bila hata kukanyaga ardhi ya nchi nyingine.

Baadhi ya wanafunzi wanaona masomo ya mtandaoni pia yana manufaa yake, kama vile kupunguza gharama za maisha ikilinganishwa na kuishi katika nchi za nje.

Wengine wanaona masomo ya mtandaoni yamekomboa muda wao binafsi, na wamekuwa na nafasi ya kufanya wanayopenda kufanya baada ya masomo. Uzuri mwingine wa masomo ya mtandaoni ni kwamba yanaweza kurudiwa mara kwa mara, hata kama wakishindwa kuelewa vizuri wakati wa masomo mubashara.