Marubani wa Kenya Airways wapata mamilioni licha ya janga la Corona
2021-03-26 18:39:09| cri

Marubani wa shirika la ndege la Kenya, Kenya Airways wanadaiwa kujiingizia mamilioni ya fedha licha ya kufanya kazi kwa masaa machache wakati huu ambapo kumekuwa na vutanikuvute kuhusu mpango wa shirika hilo kuwaachisha kazi baadhi ya wafanya kazi wake.Chama cha kutetea wafanya kazi kimesitisha hatua ya shirika hilo la ndege kuwaachisha kazi marubani 207 kati ya 414 wa shirika hilo ndani ya miaka mitatu.

Hatua hiyo imewafanya marubani wa shirika hilo kufanya kazi kwa saa 30 kwa mwezi kinyume na saa 105 zilizowekwa kisheria kutokana na janga la corona ambalo limeathiri pakubwa sekta ya usafiri kote duniani.  Ijapokuwa hivi sasa wafanyakazi wa shirika hilo wanalipwa asilimia 70 ya mshahara kutokana na janga la corona, marubani bado wanalipwa mashahara wote kwasababu shirika hilo linatakiwa kukamilisha utoaji wa malipo yote pindi litakapoanza kuimarika tena.  Mwaka jana, shirika hilo lilisema kuwa asilimia 10 ya wafanyakazi wake ni marubani wa ndege na wanachukua asilimia 45 ya mshahara wa wafanya kazi wote wa shirika hilo sawa na shilingi bilioni 6.48.  Hii inamaanisha kuwa gharama ya kumlipa rubani mmoja ni shilingi milioni 1.3 kwa mwezi ikiwa ni sawa na mshahara pamoja na marupurupu ya katibu mkuu mtendaji wa mashirika ya serikali kama vile KenGen, Kenya-Re na shirika la umeme Kenya KPLC.