Miundo mbinu ya TANESCO kuboresha
2021-04-02 16:51:58| CRI

Wizara ya Nishati nchini Tanzania imesema itaendelea kuliwezesha kifedha Shirika la Umeme nchini humo(TANESCO), ili kuboresha miundombinu kwa ajili ya kuwa na umeme wa uhakika.

Naibu Waziri wa Nishati nchini humo Stephen Byabato amesema umeme upo na unaendelea kuongezwa kupitia utekelezaji wa miradi mbalimbali ili kufikia kila mwananchi.

Aidha naibu Waziri huyo alisema serikali kupita TANESCO na REA pia inaendelea kutekeleza mradi wa kusambaza umeme katika vijiji, mitaa na vitongoji visivyo kuwa na umeme kupitia miradi mbalimbali.

Alisema kazi hizo zinajumuisha ujenzi wa njia ya umeme ya msongo wa kilovoti 0.4 umbali wa kilomita 27.5, ufungaji wa transfoma 11 pamoja na kuwaunganishia umeme wateja wa awali 669.

Ameongeza kuwa TANESCO inaendelea kuunganishia umeme wateja ambao hawajaunganishwa umeme katika mitaa na vitongoji vya Tanzania Bara ikiwamo Wilaya ya Handeni kupitia majukumu yake ya kila siku.