Wafanyabiashara Arusha wampongeza Rais Samia kuweka msimamo ukusanyaji kodi
2021-04-02 16:33:36| CRI

Wafanya biashara mkoani Arusha wamempongeza rais mpya wa Tanzania Bi Samia Suluhu Hassan kwa kuweka msimamo mzuri wa ukusanyaji kodi. Taarifa hiyo inakuja muda mchache tu baada ya rais Samia kumtaka Waziri wa Fedha, Dk Mwigulu Nchemba kutanua wigo wa ukusanyaji kodi na kuonya dhidi ya kuwaua walipa kodi kwa kufunga biashara zao, kuchukua fedha na vifaa vyao vya kazi pamoja na kufunga akaunti zao. Chama cha wafanyabiashara hao wenye viwanda na kilimo katika mkoa wa Arusha (TCCIA), Chama cha Mawakala wa Utalii (Tato) na wachimbaji wa madini vimesema kauli hiyo imerejesha amani kwa wafanyabiashara na itaongeza uwekezaji chini humo. Mkurugenzi wa kampuni ya kuuza madini ya Tanzanite forever, Faisal Shabhai amesema hatua hiyo itasaidia wafanyabiashara kuendeleza biashara zao na kulipa kodi ya Serikali lakini bila kuua biashara zao. Kampuni hiyo hivi karibuni ilipewa tuzo ya walipa kodi wazuri kwenye sekta ya biashara ya madini ya vito.