Kenya yafanyanyia ukarabati uwanja wa ndege wa Manda Lamu
2021-04-02 16:33:11| CRI

Halamashauri ya Usimamizi wa Viwanja vya Ndege nchini Kenya (KAA) imeanzisha ukarabati wa uwanja wa ndege wa Manda, Kaunti ya Lamu unaokadiriwa kugharimu serikali kima cha Sh 200 milioni.

Mradi huo ambao unahusisha ujenzi na upanuzi wa njia pamoja na mahali pa kupakisha ndege punde zinapotua umepangwa kuchukua muda wa miezi sita kukamilika.

Mkurugenzi wa KAA Ukanda wa Pwani, Peter Wafula, alisema shughuli ya ujenzi na upanuzi wa sehemu hizo za uwanja wa ndege wa Manda inaendelea baada ya kuanza rasmi mwezi Machi mwaka huu.

Bw Wafula alisema wanatarajia shughuli hiyo ya ujenzi kufikia kikomo ifikapo Agosti mwaka huu.

Afisa huyo alisema KAA iliafikia kupanua na kujenga sehemu husika ili kuwezesha ndege zaidi kutua na kupata nafasi ya kupaki kwenye uwanja huo kwa wakati mmoja.

Alisema sehemu zinazokarabatiwa kwa miaka kadhaa zimekuwa katika hali mbaya, hatua ambayo ilichangia baadhi ya kampuni za usafiri wa ndege nchini, ikiwemo Jambojet kukatiza safari zake kwenye eneo la Lamu.

Bw Wafula anasema anaamini kukamilika kwa ukarabati unaoendelea uwanjani humo kutasaidia kuvutia kampuni nyingi zaidi za ndege kuanzisha huduma zake za usafiri Lamu.