Wafanyabiashara Dodoma watakiwa kupanga bidhaa zao maeneo safi
2021-04-07 18:29:03| cri

Halmashauri ya Jiji la Dodoma nchini Tanzania limewataka wafanyabiashara kuhakikisha wanapanga bidhaa zao kwenye maeneo safi ili kulinda afya za walaji. OFISA Masoko James Yuna amesema Dodoma ni Makao Makuu ya nchi hivyo ni vyema wafanyabiashara wahakikishe maeneo wanayofanyia biashara yanazingatia afya za walaji na kikidhi soko la ushindani wa bidhaa zinazoingizwa kutoka nje ya nchi.

Aliwataka kuheshimu na kutii kanuni na taratibu katika ufanyaji biashara na kujiepusha kuvamia maeneo yasiyo rafiki ambayo hayaruhusiwi.

Alisema pamoja na uhuru walionao wa kufanya biashara wafanyabiashara wanawajibu wa kushirikiana na Jiji katika kuhakikisha maeneo yasiyo rasmi wanayaepuka na kufuata maelekezo yanayotolewa.

Kuhusu viongozi wa soko la sabasaba, Ofisa huyo aliwaomba kuhakikisha wanashirikiana na Jiji ili kuhakikisha wafanyabiashara wanafuata kanuni na maelekezo yanayotolewa.