Viwanda Kununua Maziwa Kuanzia Sh33
2021-04-07 18:30:38| cri

Wizara ya Kilimo nchini Kenya imetangaza kuwa bei ya chini zaidi ya viwanda kununua maziwa itakuwa ni Sh33. Wizara hiyo imesema hatua hii inalenga kuwakinga wafugaji dhidi ya kunyanyaswa.

Waziri wa Kilimo wa Kenya Peter Munya, amesema wasimamizi hawafai kulipa wafugaji kiwango kinachopungua Sh33 kwa kila lita ya maziwa bila kuzingatia msimu.

Alisema uamuzi huo ulifanywa baada ya kupitishwa kwa sheria ya 2021 inayosimamia sekta ya bidhaa za maziwa nchini Kenya.

Amesema bei itakuwa inafanyiwa makadirio upya kila baada ya miezi sita kwa kuzingatia hali ilivyo sokoni.

Kwa sasa, viwanda vinalipa Sh40 kwa wastani kwa kila lita ya maziwa wanayopokea lakini hii ni kwa sababu kuna upungufu wa maziwa.

Inatarajiwa uzalishaji utaongezeka hivi karibuni baada ya msimu wa mvua kuanza.

Mwaka uliopita, baadhi ya viwanda vilikuwa vikilipa hata Sh19 kwa lita ya maziwa ikidaiwa kulikuwa na kiwango kingi kupita kiasi cha maziwa sokoni.