Hali katika mkoa wa Tigray nchini Ethiopia bado ni mbaya licha ya kupelekwa kwa misaada ya kibinadamu
2021-04-08 18:24:07| Cri

Ofisi ya Umoja wa Mataifa inayoratibu Masuala ya kibinadamu imesema, misaada ya kibinadamu inaweza kupelekwa katika mkoa wa Tigray, kaskazini mwa Ethiopia, lakini mapigano yanayoendelea yanasababisha watu wengi kukimbia makazi yao, na kufanya hali kuwa mbaya zaidi.

Taarifa iliyotolewa na Ofisi hiyo imesema, maelfu ya watu wamekimbilia sehemu za mijini kutokana na mapigano yanayoripotiwa kuendelea katika baadhi ya maeneo ya mkoa huo.

Taarifa hiyo imesema, baadhi ya mashirika ya kibinadamu yameweza kuingia katika miji ya Gijet na Samre katika kanda ya kusini na kusini mashariki, ambapo yameripoti kuwa idadi kubwa ya watu katika maeneo hayo wamekimbia makazi yao.

Karibu watu milioni 2.5 katika maeneo ya mkoa wa Tigray hawajapata huduma za msingi kwa kipindi cha miezi mitano iliyopita tangu mapigano yalipotokea.