Rais wa Rwanda azilaumu baadhi ya nchi kwa kukataa kuwakamata washukiwa wa mauaji ya kimbari
2021-04-08 10:21:18| CRI

 

 

Rais wa Rwanda Paul Kagame amezilaumu baadhi ya nchi ikiwemo Ufaransa, kwa kushindwa kuwafikisha washukiwa wa mauaji ya kimbari ya Rwanda mbele ya sheria.

Akizungumza jana katika kumbukumbu ya miaka 27 tangu kutokea kwa mauaji ya kimbari nchini humo mwaka 1994 dhidi ya Watutsi, rais Kagame amesema washukiwa wa mauaji hayo wamepewa hifadhi, na maombi ya Rwanda ya kuwarejesha washukiwa hao yamekataliwa katika nchi kadhaa ikiwemo Ufaransa. Ameongeza kuwa, baadhi ya kesi zimeendeshwa kwa karibu miaka 15 katika nchi za bara la Ulaya na Afrika, bila ya hukumu kutolewa.

Mapema siku hiyo, rais Kagame na mkewe Mama Jeannete Kagame pamoja na balozi wa Jamhuri ya Congo, Guy Nestor Itoua, pamoja na wawakilishi wa wahanga wa mauaji hayo waliweka taji la maua katika Mnara wa Kumbukumbu ya Mauaji ya Kimbari mjini Kigali, ambapo zaidi ya watu 250,000 waliouawa wamezikwa.