Kenya yaunda bodi ya kusimamia usalama wa chanjo ya COVID-19
2021-04-08 10:21:44| CRI

 

 

Kenya imetangaza kuunda bodi huru ya kusimamia usalama wa chanjo ya virusi vya Corona, huku kukiwa na mwitikio mkubwa wa umma wa kupata chanjo hiyo.

Mwenyekiti wa kikosikazi kuhusu chanjo nchini humo, Willis Akhwale amesema, bodi hiyo itashughulikia athari mbaya za chanjo hiyo kwa makundi yaliyolengwa katika awamu ya kwanza ya chanjo dhidi ya virusi vya Corona.

Amesema lengo ni kuhakikisha athari mbaya ya chanjo hiyo inaripotiwa, isipokuwa kwa watu ambao wameripoti athari kidogo za chanjo hiyo, kama uchovu na maumivu ya kichwa.

Akhwale amesema, hakuna ripoti zozote zinazohusisha kesi za kuganda kwa damu nchini Kenya kama ilivyo katika nchi nyingine duniani baada ya kupata chanjo hiyo.

Kwa mujibu wa Wizara ya Afya nchini humo, watu 339,893 wamepata dozi za chanjo ya AstraZeneca, na 228 wamepokea chanjo ya Sputnik V ya Russia.