Wazazi watafuta njia mbalimbali kuwasaidia watoto wanaochoka na masomo
2021-04-14 17:07:44| Cri

Takwimu zimeonesha kuwa, asilimia 46 ya wanafunzi wa shule za msingi na za sekondari nchini China hawana hamu ya kujifunza, asilimia 33 wamechoka na masomo, na ni asilimia 21 tu wanapenda sana kujifunza, hali ambayo imeonesha kuwa “uchovu wa kujifunza” ni jambo la kawaida. Wazazi wanaosumbuliwa na hali hii pia wanatafuta njia mbalimbali za kuwasaidia watoto wao.

Hivi karibuni huko Hangzhou, video moja iliyosambaa mtandaoni imefuatiliwa sana na watu. Katika video hiyo, mvulana mwenye umri wa miaka 15 alisema amechoka sana kusoma, hivyo baba yake akampeleka kubeba matofali katika eneo la kiwanja cha ujenzi. Baada ya kupata uzoefu mgumu akiwa mfanyakazi wa ujenzi, alisema analotaka ni kuendelea na masomo. 

Kwingineko, huko mji wa Shenyang, mkoani Liaoning, mtoto mmoja wa kike aliyesoma mwaka wa pili katika shule ya msingi hakupenda kusoma, na mama yake alimpeleka kukusanya taka. Bila ya kutarajiwa, kutokana na uzoefu huo, mtoto wake sio tu alianza kujifunza kwa hiari, pia alimwuliza mama yake kama ataweza kuacha kukusanya taka ikiwa atashika nafasi tatu za mwanzo katika mtihani.