Waziri wa Sudan Kusini akosolewa kwa kumlazimisha mkewe kuondoka katika mechi ya Ligi ya Soka ya nchi hiyo
2021-04-26 20:20:44| Cri

Shirikisho la Soka la Sudan Kusini SSFA limemkosoa vikali waziri mmoja wa serikali kutokana na kuvuruga mechi moja ya ligi ya taifa ya wanawake kwa kumtaka mkewe ambaye ni mchezaji wa soka kuondoka kwenye mechi hiyo.

Ripoti zinasema, Aluel Garang anayejulikana kama Aluel Messi alichezea timu ya Aweil Women dhidi ya timu ya Juba Super Stars wikiendi iliyopita, wakati mumewe ambaye ni waziri wa mambo ya kibinadamu na usimamizi wa maafa Peter Mayen Manjongdit alipofika uwanja wa Aweil Freedom na kusimamisha mechi hiyo kwa kumlazimisha mkewe kuondoka.

Katika taarifa iliyotolewa ikithibitisha vurugu hiyo, shirikisho la SSFA limeeleza kuangushwa na hatua hiyo ya ofisa wa serikali.

Kwa mujibu wa vyombo vya habari vya huko, waziri huyo alivamia uwanja wa soka huku akiwataka waandalizi kusimamisha mechi hiyo na kumtaka mkewe kuondoka. Waziri huyo hakufurahi kutokana na mkewe kumwachia mtoto mchanga wa miezi mitatu nyumbani na kujiunga na wenzake katika mechi.

Imefahamika kwamba waziri huyo aliambiwa asubiri, lakini alishindwa kuvumilia na kufyatua risasi hewani na kuvuruga mechi hiyo. Baadaye mechi hiyo ilisimamishwa na kumruhusu waziri huyo kurudi nyumbani pamoja na mkewe.