Mama anagundua bi harusi wa mwanawe ni binti yake aliyepotea muda mrefu
2021-04-27 16:07:08| Cri

Je utafanya nini endapo siku ya harusi unagundua kuwa mke wa mtoto wako wa kuasili kuwa ni binti yako aliyepotea muda mrefu sana?

Mwanamke mmoja aligundua kuwa bi harusi wa mtoto wake ni binti yake aliyepotea muda mrefu sana wakati walipokuwa kwenye siku yao ya harusi nchini China.

Mwanamke huyo aliripotiwa kumtambua binti yake, ambaye alikuwa ametengana naye miaka mingi iliyopita, kwa kuona alama ya kuzaliwa mkononi mwake siku ya sherehe. Alilazimika kuwauliza wazazi wa bi harusi kama binti yao alikuwa ameasiliwa.

Wazazi walishangazwa na swali hilo kabla ya kusema kwamba walikuwa wamemuasili mtoto huyo baada ya kumpata kando ya barabara zaidi ya miaka 20 iliyopita.

Bi harusi na mama yake walionekana wakilia na kukumbatiana wakati walipokutana bila kutarajia huko Suzhou, mkoa wa Jiangsu mnamo Machi 31. Hata hivyo harusi iliweza kuendelea baada ya kubainika kuwa mtoto wa mwanamke huyo alikuwa ameasiliwa, ikimaanisha maharusi hao walikuwa hawahusiani kabisa.

Mwanamke huyo aliripotiwa kuamua kuasili mtoto wa kiume baada ya kumtafuta binti yake bila mafanikio kwa miaka mingi. Baada ya kusikia mkasa huo, bi harusi aliangua kilio na kuelezea wakati huo wa kukutana na mama yake mzazi kama "ni wa furaha kuliko siku ya harusi yenyewe".

Harusi iliweza kuendelea licha ya habari hiyo ya kushangaza na wanandoa hao walikula kiapo.