Mchina wa kwanza anayejitolea kugandishwa mwili wake baada ya kufariki asajiliwa
2021-04-27 15:51:38| Cri

Bibi Zhan Wenlian ni mtu wa kwanza aliyejitolea kugandishwa mwili wake baada ya kufariki dunia nchini China, na mpaka sasa mwili wake umehifadhiwa katika nyuzi joto 196 chini ya sifuri kwa siku 1,345.

Mume wake Gui Junmin amesema uamuzi huo wa kuhifadhi mwili wa mke haulengi kutoa mchango kwa sayansi ya kimatibabu, bali unatokana na kuwa hataki kuagana naye.

Mwaka 2015, marehemu Zhan Wenlian aligunduliwa kuwa na saratani ya mifupa ngazi ya tatu, na aliamua kuchangia mwili wake kabla ya kuaga dunia, wakati huo ndipo Bw. Gui Junmin alifahamu teknolojia ya kugandisha mwili wa marehemu kwa matumaini ya kufufuliwa katika siku za baadaye.

Ingawa uwekezeno wa kufufuliwa bado ni makadirio ya kinadharia, lakini ulikuwa kama mshumaa wa mwisho uliomletea matumaini Bw. Gui.

Baada ya kupata kibali chake mwenyewe, Bibi Zhan Wenlian alitangazwa kufariki dunia Mei 8 mwaka 2015.

Baada ya kufanyiwa upasuaji kwa saa 55, mwili wa marehemu uliwekwa kwenye mtungi mkubwa wa majimaji ya Nitrogen yenye nyuzi joto 196 chini ya sifuri, na Bw. Gui Junmin akaanza subira ya muda mrefu.

Imefahamika kuwa hivi sasa kuna taasisi nne tu zenye uwezo wa kugandisha mwili kote duniani, mbili nchini Marekani, moja nchini Russia na nyingine nchini China. Mpaka sasa miili ya watu zaidi ya 100 kote duniani imehifadhiwa kwa kugandishwa, lakini bado hakuna mtu yeyote aliyefanikwa kufufuliwa.