Mzazi wa mwanafunzi ajenga daraja la kuvuka barabara
2021-04-28 18:21:34| Cri

Mama wa mwanafunzi kutoka Shule ya sekondari ya Kaunti ya Xiayi katika mji wa Shangqiu, mkoani Henan, aligharamia RMB yuan mamilioni, kujenga daraja kwa ajili ya wanafunzi kuvuka barabara. Daraja hilo liko katika barabara ya Kongzu ambayo ni barabara muhimu katika kaunti hiyo. Kila siku magari mengi yanapita hapo, na wakati wanafunzi wa shule ya sekondari ya Xiayi wanapotoka nje baada ya masomo, kunakuwa na msongamano mkubwa wa magari na watu barabarani, na usalama wa wanafunzi barabarani unawafanya wazazi wawe na wasiwasi mkubwa. Mbali na hayo, kila mvua zinaponyesha, barabara hiyo inajaa maji, haswa wakati wa majira ya joto.

Bibi Meng alizungumzia jambo hilo alipowasiliana na mkuu wa shule ya sekondari hiyo. Kutokana na pendekezo la mkuu wa shule, Bibi Meng aliamua kugharamia kujenga daraja la kuvuka barabara baada ya kuidhinishwa na idara zinazohusika za serikali. Kitendo hicho kimepongezwa na watu wengi, lakini wengine wanauliza kwa nini mamlaka ya elimu na idara za upangaji wa uchukuzi hazikuchukua hatua yoyote? Elimu si jambo dogo, na inapaswa kuzingatiwa kwa vitendo halisi.