Suala la vijana kupata tattoo
2021-05-06 15:40:08| Cri

Tarehe 14 Aprili mwaka huu, kijana Liu Ke ambaye hajatimiza miaka 17 aliweka picha zake kwenye mtandao na kuandika kwamba “nimechagua njia hii, nitaimaliza hata kama nitatembea kwa magoti”, kabla ya kukamatwa na polisi kwa tuhuma za kuzusha varangati. Uchunguzi wa polisi unaonesha kuwa kijana huyo alishiriki kwenye kesi mbili za varangati, ambazo zilizosababisha watu kadhaa kujeruhiwa. Kijana Liu Ke na wengine zaidi ya kumi waliokamatwa kuhusiana na kesi hiyo wote wana tattoo kwenye sehemu mbalimbali za miili yao.

Naibu mwendesha mashtaka mkuu wa wilaya ya Shuyang mkoani Jiangsu Ye Mei aliyeshughulikia kesi ya Liu Ke, amesema vijana wengi wanaweka tatoo kwenye miili yao kwa kuiga wenzao, na kuona kuwa tattoo zinaonesha umwamba na ujanja wao na ziko poa sana.

Ofisa huyo amesema tattoo si kama tu zinaleta madhara kwa miili ya vijana, na bali pia zinatoa athari hasi kwa mustakbali wao. Hivi sasa watu wenye tattoo hawaruhusiwi kusajiliwa katika jeshi na polisi, na wala hawawezi kuajiriwa na serikali kama watumishi wa umma. Pia wanaweza kukumbwa na masumbufu mbalimbali kwenye kujiunga na shule, kupata ajira na kutafuta wachumba.