“Blind Boxes” za vitu vya kuchezea zanyakua soko kubwa la vijana China
2021-05-11 20:55:07| Cri

“Blind Boxes” ambazo ni njia ya kufanya manunuzi ya kubahatisha zimekuwa maarufu sana miongoni mwa vijana wa China, na kuwapatia utajiri mkubwa wazalishaji wa vitu vya kuchezea.

Kwa mujibu wa ripoti ya utafiti wa soko iliyotolewa na Qianzhan Intelligence, Soko la Blind Boxes lilikuwa na thamani ya dola za kimarekani bilioni 1.14 mwaka 2019, na linakadiriwa kufikia dola za kimarekani bilioni 4.66 kabla ya mwaka 2024.

Mwanzilishi wa kundi la Popmart International ambalo limeorodheshwa rasmi kwenye soko la hisa la Hongkong Disemba 11 mwaka jana, Wang Ning, na mke wake wanamiliki asilimia 49.8 ya kampuni hiyo, ambayo mapato yaliongezeka mara 300 kutokana na mauzo ya Blind Boxes.

Ikifanana na kukusanya kadi za Baseball, vijana wananunua blind boxes ili kukusanya aina mbalimbali tofauti za vitu vya kuchezea vyenye ukubwa wa ngumi vilivyoko ndani ya visanduku hiyo. Vijana wanasema raha ya kununua Blind Boxes ni kwamba huwezi kujua utapata nini kabla ya kufungua, lakini ukitaka kukusanya aina zote, lazima uendelee kununua.

Chombo cha habari cha taifa kilikosoa njia hiyo, na kuitaja kama mchezo wa kamari na kuwatahadharisha vijana dhidi ya uraibu wa mchezo huo, na pia kimetoa wito kwa idara husika kuimarisha usimamizi wa sekta hiyo.