SOKA: Eden Hazard Afikiria Kurejea Chelsea Baada ya Masaibu Kumzonga Real Madrid
2021-05-25 18:24:20| cri

Eden Hazard anaripotiwa kufikiria kurejea ugani Stamford Bridge baada ya kukumbana na masaibu Real Madrid. Hazard hajawa na wakati mzuri Real Madrid tangu kujiunga na klabu hiyo ya ndoto yake mwaka 2019. Misururu ya majeraha imemzuia Mbelgiji huyo kusakata soka katika jiji kuu la Uhispania ambapo ameshiriki mechi 10 pekee za La Liga msimu huu. Mbelgiji huyo anawazia kuondoka Madrid msimu huu akilenga kurejea Chelsea. Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 30, alifurahia taaluma yake na Blues kwa miaka saba na kuwasaidia kutwaa mataji ya Ligi Kuu, Kombe la FA na UEFA. Mapema mwezi huu, ripoti kutoka Uhispania zilidai kuwa Madrid wanapania kumuweka mnadani winga huyo na kuwasajili wachezaji wapya. Nyota wa Paris Saint-Germain Kylian Mbappe na Dortmund Erling Haaland tayari wameanza kutupiwa ndoano lakini Madrid watalazimika kuuza baadhi ya wachezaji wao wakuu kupata pesa za kufadhili uhamisho. Hali hii inayozingira hatima ya mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 30, inakuja baada ya kuwaghadhabisha mashabiki wa Madrid kwa kuonekana akichekea na wachezaji wa Chelsea.