Kaseke aipeleka Yanga nusu fainali kombe la Shirikisho
2021-05-26 18:18:31| cri

Mabingwa wa zamani wa kombe la Shirikisho nchini Tanzania, klabu ya Yanga imefanikiwa kutinga hatua ya nusu fainali ya michuano ya kombe hilo baada ya kuifunga timu ya Mwadui mabao 2-0 yaliyofungwa na kiungo wake Deus Kaseke kwenye dimba la CCM Kambarage mkoani Shinyanga. Kaseke amefunga mabao hayo na kuendelea kuibeba Yanga kwenye mabega yake kwani ukiondoa mabao hayo mawili ya kuivusha timu, kaseka ana mabao 6 kwenye VPL, bao moja nyuma ya Yacouba Sogne mwenye mabao mengi, mabao 7 kwenye VPL. Kaseka amezidi kuonesha kuwa yeye ni lulu kwenye kikosi hicho cha Wananchi kwa kufikisha bao lake la 9 msimu huu kwenye michuano yote ikiwa ni idadi yake ya mabao mengi zaidi kwenye msimu mmoja akiwa na Yanga.

Ushindi huo unaifanya Yanga kukutana na klabu ya Biashara United Mara kwenye hatua ya Nusu fainali ya michuano hiyo huku Mwadui amehitimisha msimu wake kwa kushuka daraja kutoka Ligi kuu Bara na kwenda ligi daraja la kwanza.