Simba kuvuta vifaa vinne vya CAF
2021-05-26 18:20:02| cri

Katika kuhakikisha msimu ujao wanafanya vema kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika, Kocha Mkuu wa Simba, Mfaransa, Didier Gomes amewaambia mabosi wake kuwa anahitaji wachezaji wanne pekee kutoka nje ya nchi. Hiyo ikiwa ni siku chache tangu timu hiyo iondolewe na Kaizer Chiefs katika hatua ya Robo Fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika, michuano inayosimamiwa na Shirikisho la Soka Afrika (CAF). Simba imeondolewa na Kaizer Chiefs baada ya kufungwa jumla ya mabao 4-3 ambapo ugenini ilifungwa 4-0, kabla ya juzi kurejeana kwenye Uwanja wa Mkapa, Dar es Salaam na kufanikiwa kupata ushindi wa 3-0. Kwa mujibu wa taarifa, Gomes ametoa mapendekezo hayo ya usajili baada ya kukutana na mabosi, akitaka beki wa kati, kiungo mchezeshaji, winga na mshambuliaji. Mtoa taarifa huyo alisema kuwa usajili wa wachezaji kutoka nje ya nchi una lengo la kutengeneza kikosi chenye ubora kitakachofanya vema katika michuano ya kimataifa baada ya msimu huu kutolewa hatua ya robo fainali.