SOKA: Zidane aipa mkono wa kwaheri Real Madrid
2021-05-28 15:39:13| cri

Klabu ya Real Madrid ya Hispania imethibitisha kuwa Kocha Zinedine Zidane amejiuzulu nafasi yake ya ukocha ndani ya kikosi hicho. Taarifa hiyo imekuja baada ya kikosi hicho kuukosa ubingwa wa Ligi Kuu nchini Hispania La Liga kwa tofauti ya alama mbili dhidi ya majirani zao kutoka jiji la Madrid klabu ya Atletico Madrid. Zidane ameifundisha Real Madrid katika vipindi viwili tofauti, awamu ya kwanza ilikuwa Januari 4, 2016 mpaka Mei 31, 2018, ambapo alikiongoza kikosi hicho kwenye michezo 149 na kushinda jumla ya mataji 9 ikiwemo ubingwa wa ligi kuu Hispania La Liga na alitwaa ubingwa wa klabu bingwa barani ulaya mara 3 mfululizo. Alirejea kwa mara ya pili kuanzia Machi 11 2019 mpaka Mei 27, 2021, na katika awamu hii amefanikiwa kushinda mataji mawili tu.