Wanandoa wa China watimiza ndoto ya kueneza Tiba ya Jadi ya Kichina nchini Afrika Kusini
2021-06-18 09:32:12| CRI

Karibu na mtaa wa China Town mjini Johanesburg, Afrika Kusini, kuna hospitali moja ya matibabu ya jadi ya kichina (TCM). Ingawa hospitali hiyo si kubwa sana, lakini kila siku wagonjwa wengi wanakwenda kutafuta matibabu, wakiwemo maofisa waandamizi, watu mashuhuri na nyota wa filamu wa Hollywood. Mafanikio ya hospitali hiyo yote yanatokana na ndoto ya wanandoa madaktari wa China ya kueneza matibabu hayo ya asili kutoka nchini mwao.

Bw. Xu Youqiang na Bi. Sun Qingfu ni wanafunzi wenza wa TCM waliojiunga chuo kikuu cha matibabu ya jadi ya kichina cha Chengdu mwaka 1977, na baada ya kuhitimu walifanya kazi kwa miaka kadhaa katika taasisi za matibabu nchini China, kabla ya kwenda Afrika Kusini mwaka 1991.

Wakikumbuka machungu waliyopitia, wanandoa hao wanasema changamoto ya kwanza ilikuwa ni lugha, na mwanzoni waliweza tu kuwasiliana na wagonjwa kwa ishara. Bi. Sun Qingfu anasema, wakati ule hawakuwa na pesa, na walitegemea mapato yanayotokana na biashara ya uchuuzi mitaani kuendeleza huduma za zahanati yao. Hata hivyo, zahanati hiyo ililazimika kuhama mara kadhaa baada ya vitendo vya wizi na uporaji kutokea mara kwa mara.

Katika miaka ya 90 karne iliyopita, watu wa Afrika Kusini hawakuwa na ufahamu kuhusu matibabu ya jadi ya kichina. Bi. Sun bado anakumbuka kulikuwa na mwanamke mmoja ambaye alitishia kuwafungulia mashtaka wanandoa hao baada ya kupewa tiba ya vikombe ya kichina (Cupping Therapy) kwa kuwa aliona ngozi yake imebadilika rangi na kuonekana kuwa na majeraha.

Hata katika wakati huo mgumu, wanandoa hao hawakukata tamaa. Bibi Sun alisema sababu ni kwamba, walishikilia ndoto yao ya kueneza Matibabu ya Jadi ya Kichina (TCM), na kuwafahamisha watu wa Afrika Kusini kuwa matibabu hayo ni mbinu yenye ufanisi ya kutibu magonjwa. Bibi Sun anaona kuwa, Waafrika Kusini wanapenda tiba asilia, na tiba ya jadi ya kiafrika na tiba ya kichina zinaweza kupata maendeleo kwa pamoja kupitia kuwasiliana na kufundishana.

Baada ya kushindwa mara tatu kufungua zahanati, wanandoa hao waliamua kufanya biashara kwanza ili kupata fedha za kutosha kuanzisha hospitali yao.

Mwaka 1998, wanandoa hao hatimaye walinunua nyumba moja na kufungua rasmi hospitali yao ya tiba ya jadi ya kichina. Baada ya juhudi za miaka mingi, hospitali hiyo imepata umaarufu, na wagonjwa wengi wanatoka nchi nyingine za Afrika kama vile Namibia, Somalia, Ethiopia na Msumbiji.

Nyota wa Hollywood Gwyneth Paltrow pia ni mmoja wa wateja wa mara kwa mara wa hospitali hiyo. Kila mara anapofika Afrika Kusini, Bibi Paltrow ataenda hospitali hiyo kupata tiba ya vikombe ili kupunguza maumivu ya mgongo. Bibi Sun amesema, picha ya Bibi Paltrow akiwa na alama za kupewa tiba ya vikumbe mgongoni ilichapishwa kwenye magazeti ya Afrika Kusini, na kuongeza zaidi umaarufu wa hospitali yao. Ameongeza kuwa hawakuwahi kufanya matangazo ya kibiashara, na umaarufu wao unatokana na sifa wanayopata kutoka kwa wateja.

Kwenye kipindi cha janga la Corona, wanandoa hao waliandaa shughuli tatu za kusambaza dawa ya mitishamba ya kichina ya kuongeza kinga mwili, na kutibu mamia ya wagonjwa wenyeji kwa njia ya mtandao. Wamesema wanatumai kuwa tiba ya jadi ya kichina inaweza kutumiwa na watu wengi zaidi nchini Afrika Kusini.

Mbali na kuwafahamisha watu wa Afrika Kusini kuhusu tiba ya kichina kwa kutumia ustadi wao mzuri wa matibabu, wanandoa hao pia walifanya juhudi kubwa kuhimiza tiba ya jadi ya kichina kuingia kwenye mfumo wa matibabu wa nchini humo. Mwaka 1998 na 1999, wabunge wa Afrika Kusini waliwasilisha miswada ya sheria kuhusu tiba ya jadi ya kichina kwa miaka miwili mfululizo, lakini yote ilikataliwa. Bw. Xu Youqiang aligundua kuwa miswada hiyo ilinukuu kauli zilizotolewa na Jumuiya tofauti za TCM, ambazo baadhi zinakinzana, na hivyo watu wa Afrika Kusini hawakuzielewa vizuri.

Katika hali hiyo, Bw. Xu Youqiang alidhamiria kuanzisha shirikisho la pamoja la tiba ya jadi ya kichina, ili kutoa sauti ya pamoja na kujenga kwa pamoja sifa na hadhi ya TCM nchini Afrika Kusini. Kutokana na juhudi alizofanya Bw. Xu Youqiang, Shirikisho la TCM la Kusini mwa Afrika lilianzishwa rasmi, na Bi. Su Qingfu kuwa mwenyekiti wake. Wanandoa hao waliwasiliana na wabunge wa Afrika Kusini kupitia shirikisho hilo, ambao waliwasilisha bungeni kwa mara nyingine tena muswada wa sheria kuhusu Tiba ya Kichina. Hatimaye, mwaka 2000, tiba ya jadi ya kichina ilihalalishwa rasmi nchini humo. Baadaye, wanandoa hao pia walisaidia kuandikisha aina zaidi ya 800 za dawa za mitishamba za kichina, na hivyo kujenga hadhi ya TCM na dawa ya jadi ya kichina nchini Afrika Kusini.

Wanandoa hao wamesema, katika hatua ijayo, wanapanga kuunganisha TCM na nyanja ya Bioinformatics, ili kutafuta nadharia ya TCM inayoeleweka na kukubalika zaidi duniani, na kuifanya tiba ya kichina kuwanufaisha watu wengi zaidi.