China inaendelea kushirikiana na Tanzania kwenye miradi inayogusa maisha ya watu moja kwa moja
2021-07-07 16:04:28| cri

China inaendelea kushirikiana na Tanzania kwenye miradi inayogusa maisha ya watu moja kwa moja_fororder_VCG111222974815

Na Fadhili Mpunji

Hivi karibuni Mkuu wa Chuo Cha Usafirishaji cha Tanzania (NIT) Prof Zacharia Mganilwa, alisema mabadiliko yanayoendelea kutokana na upanuzi wa chuo hicho yatainua hadhi na ubora wa chuo hicho na kuwa chuo kikuu cha kisasa. Mabadiliko yanayoendelea kwenye upanuzi wa chuo hicho, ni sehemu ya utekelezaji wa ushirikiano kwenye sekta ya elimu kati ya China na nchi za Afrika. Upanuzi wa Chuo hicho unatajwa kugharimu zaidi ya dola za kimarekani milioni 62, Tanzania ikiwa mmoja wa wanufaike wa mpango wa kujenga vyuo vikuu vitano vya mambo ya usafirishaji barani Afrika.

 

Mara nyingi tunapozungumzia ushirikiano kati ya China na Tanzania, watu wengi wanakumbuka zaidi ujenzi wa reli ya TAZARA, na katika siku za hivi karibuni watu wamekuwa wakiangalia zaidi ujenzi wa miundombinu ya usafiri. Lakini ukweli ni kuwa toka zamani, China haijajikita kwenye ujenzi wa miundombinu peke yake. Hata wakati wa ujenzi wa reli ya TAZARA, kulikuwa na wahandisi wa China waliokuwa kwenye maeneo mengine. Kulikuwa na wale waliojenga kiwanda cha nguo cha Urafiki cha Ubungo, na kulikuwa na wale waliokuwa wakijenga viwanda vya zana za kilimo, kama vile UFI cha Ubungo, na ZZK cha Mbeya. Viwanda hivi viliwanufaisha wakulima moja kwa moja.

 

Siku zote China huwa inasema haitawasahau ndugu zake wa Afrika, hata ikiwa na maendeleo makubwa kiasi gani. Hii ni kauli ambayo China imekuwa inairudia mara kwa mara. Lakini je, tukiangalia hii China ya leo, ni kweli inafanya kama inachosema? Tukiangalia hali ya Tanzania tunaweza kuona kuwa kauli hii ina ukweli ndani yake, lakini manufaa yake hayaishii Tanzania tu.

Kwanza, tukianza kuangalia Chuo cha Usafirishaji NIT, hiki ni chuo ambacho baada ya kukamilika kitakuwa moja ya vyuo vitano vikubwa vya usafirishaji barani Afrika. Hii ni fursa nzuri kwa Tanzania, kwani chuo pia kitaweza kuvutia wanafunzi kutoka nchi nyingine za Afrika. Profesa Mganilwa amesema nchi za jirani kama Kenya, Uganda, Kongo DRC, Burundi, Rwanda, Uganda, Malawi na Zambia pia zitanufaika, kwa kuleta wanafunzi wao kufuata kozi za uchukuzi.

 

Pili tukiangalia kwenye sekta ya afya, sidhani kama kuna mjadala kuwa hospitali ya magonjwa ya moyo ya Jakaya Kikwete ni moja ya hospitali za kisasa barani Afrika. Hospitali hii licha ya kuwa imeboresha huduma za matibabu ya moyo nchini Tanzania, pia imeiondolea Tanzania mzigo mkubwa wa kifedha wa kugharamia matibabu nje ya nchi. Lakini hii sio kwanza Tanzania tu, hata nchi za jirani pia zinaweza kunufaika na huduma za hospitali hiyo. Lakini mbali na hayo China pia imekuwa ikishirikiana na Tanzania kuimarisha uwezo kwenye sekta ya afya kwa kutoa mafunzo kwa watanzania, ili wao wenyewe waweze kusimamia hospitali hiyo.

 

Lakini mbali na miradi kama hii, kuna miradi mingine mikubwa inaendelea ambayo haiko kwenye sekta ya ujenzi wa miundo mbinu ya usafiri na inanufaisha watu wengi. Nchi Tanzania tumeona miradi kwenye sekta ya kilimo kama vile mradi wa ushirikiano wa kilimo wa Morogoro, unaosaidia wakulima kuongeza uzalishaji wa mahindi kwa hekta, au mradi wa mashamba makubwa ya mpunga kama mradi wa kilimo cha mpunga wa Kapunga. Hii ni baadhi tu ya miradi inayotekelezwa na China na kuwanufaisha watu, lakini si miradi ya reli au barabara.