China yaendelea kutoa fursa kwa nchi za Afrika Mashariki kujitangaza kwenye soko la China.
2021-07-08 10:22:08| cri

China yaendelea kutoa fursa kwa nchi za Afrika Mashariki kujitangaza kwenye soko la China._fororder_1

China yaendelea kutoa fursa kwa nchi za Afrika Mashariki kujitangaza kwenye soko la China._fororder_2

Na Fadhili Mpunji

Kenya, Tanzania na Rwanda zimeendelea na juhudi zao katika kutanganza vivutio vyake katika soko la China ikiwa ni pamoja na vivutio vya utalii, sanaa za mikono, na hata bidhaa za kilimo kama kahawa. Kwenye hafla moja iliyofanyika mashariki mwa mji wa Beijing na kutangazwa moja kwa moja kwa milioni ya wananchi wa China kupitia televisheni ya Hunan, mabalozi wa Kenya, Tanzania na Rwanda walikuwa ukumbini na kutumia fursa hiyo kutangaza vivutio hivyo.

Hii si mara kwanza kwa nchi za Afrika Mashariki kutumia njia hii kujitangaza kwenye soko la China. Mara kadhaa balozi za nchi hizi zimekuwa zikitumia njia hii na njia ya Online Streaming kutangaza bidhaa zinazozalishwa katika nchi zao, na wakati mwingine watazamaji huagiza bidhaa hizo moja kwa moja wakiwa wanafuatilia matangazo. Ubunifu huu umekuwa unatumika nchini China kuhimiza biashara kati ya maeneo ya vijijini na mijini, na ulikuwa na manufaa makubwa sana wakati wa janga la COVID-19.

Kwenye maonyesho hayo kumekuwa na mambo ya kuvutia, ambayo yaliwashangaza watu waliokuwa ukumbini na wengine wengi waliokuwa wakifuatilia moja kwa moja kwa njia ya televisheni.  Balozi wa Kenya nchini China Madam Sarah Selem, aliwaacha midomo wazi mamia ya vijana wa China waliokuwa ukumbini, pale alipowafahamisha kuwa simu zao aina ya iPhone zina uwezo wa kusikiliza maagizo kwa njia ya sauti unaofahamika kwa jina la SIRI, ambalo ni neno la Kiswahili. Lakini sio hilo tu, bali pia walishangaa kufahamishwa kuwa ajabu la nane la dunia, ambalo ni uhamiaji mkubwa wa wanyamapori kati ya Tanzania na Kenya, upo kwenye eneo la Afrika Mashariki.

Kutokana na changamoto ya COVID-19, shughuli nyingi zinazohusu kusafiri kati ya China na nchi za Afrika zimepungua sana. Hata hivyo hali hii haijapunguza shughuli za kujitangaza kwa nchi za Afrika nchini China. China imekuwa inaendelea kuziwezesha nchi za Afrika kujitangaza na kuuza bidhaa zao nchini China, licha ya mazingira magumu ya usafiri kutokana na vizuizi vya karantini vya kukabiliana na janga la COVID-19. Balozi za nchi za Afrika mashariki zinatumia vizuri fursa hii kujitangaza nchini China.

Mbali na ngoma za Rwanda na Tanzania, kulikuwa na sanaa nyingi za mikono kutoka nchi za Afrika Mashariki zilizoonyesha kwenye hafla hiyo. Ofisa wa mambo ya utamaduni wa ubalozi wa Kenya nchini China, alitumia muda huo kutangaza utalii wa Kenya, kahawa ya Kenya na hata sanaa za mikono kama sanamu na vinyago. Ofisa wa Tanzania alitangaza madini ya Tanzanite, kahawa, viungo kutoka Zanzibar, vinyago, korosho na mvinyo.