Waziri mkuu wa China asisitiza udhibiti wa mafuriko, na ufunguaji mlango katika sekta ya fedha
2021-07-22 08:58:50| CRI

Waziri mkuu wa China Bw. Li Keqiang jana Jumatano alitoa wito wa kuimarisha udhibiti wa mafuriko na misaada ya maafa kwenye maeneo yaliyoathirika na kuhimiza ufunguaji mlango kwenye sekta ya fedha.

Bw. Li alitoa kauli hiyo alipoongoza mkutano wa Baraza la Serikali, ambao pia uliweka hatua za kurahisisha biashara ya kuvuka mpaka na kuboresha mazingira ya kibiashara kwenye bandari.

Bw. Li alisema China inapaswa kutenga fedha na vifaa kuusaidia mkoa wa Henan kwenye kazi ya uokoaji, uhamishaji wa watu na utoaji wa misaada ya maafa. Pia alisisitiza mipango ya mwitikio wa dharura kwa miundombinu ya uchukuzi na kuzuia majanga mengine yanayoambatana na mafuriko.

Kuhusu suala hilo, Bw. Li pia alitoa wito wa kufanya juhudi kuimarisha ufuatiliaji wa hali ya hewa na kuifanyia ukarabati miundombinu ya maji.

Akizungumzia ufunguaji mlango wa sekta ya fedha, Bw. Li amesema unatarajiwa kuwa kiini cha kuvutia uwekezaji wa kigeni na kufikia viwango vya kimataifa.