Marafuku kwa wenyeji kula matangani
2021-07-26 07:34:02| cri

Kamishna wa Kaunti ya Bungoma nchini Kenya Bw Samuel Kimiti amepiga marufuku kula kwa matanga akisema agizo hilo linanuia kupunguza msambao wa virusi vya corona.

Bw Kimiti alionya kuwa mazishi yataruhusiwa tu kufanyika kwa muda wa saa 72 kama ilivyoamrishwa na serikali.V ilevile, waombolezaji ni 50 pekee kujumuisha jamaa na marafiki wa karibu wa mwendazake.

Aliongeza kuwa wanaofanya kazi masaa ya kafyu watakamatwa na kushtakiwa. Alionya watu kuuchukulia ugonjwa huo kwa tahadhari kwa kuwa wengi wamepoteza wapendwa wao kupitia virusi hivyo.

Bw Kimiti aliwaomba wakaazi hao kushirikiana na serikali kwa kuzingatia kanuni zilizotolewa kama vile, kuosha mikono kila mara, kuvaa barakoa na kutokaribiana ili kupambana na janga hilo.Aliwaonya polisi ambao wanachukua hongo kutoka kwa wamiliki baa na kuwaruhusu kufanya kazi wakati wa kafyu kuwa watachukuliwa hatua.

Katika siku mbili zilizopita, polisi wamewakamata waendeshaji bodaboda pamoja na wamiliki baa wengi waliovunja kanuni za kafyu.