Rais wa Marekani asema nchi hiyo kumaliza majukumu yake ya kijeshi nchini Iraq mwisho wa mwaka huu
2021-07-27 08:48:06| cri

Rais Joe Biden wa Marekani amesema jana kuwa, jeshi la nchi hiyo litamaliza majukumu yake ya mapambano nchini Iraq mwishoni mwa mwaka huu.

Akizungumza katika Ikulu ya Marekani akiwa na waziri mkuu wa Iraq Mustafa al-Kadhimi aliyeko ziarani nchini Marekani, rais Biden amesema baada ya mwaka huu, majukumu ya jeshi la Marekani nchini Iraq yatakuwa ni kutoa mafunzo, kutoa msaada, na kusaidia kupambana na kundi la IS kama itakavyotakiwa.

Ameongeza kuwa, ushirikiano katika kupambana na ugaidi utaendelea hata pale jeshi hilo litakapoanza kutekeleza majukumu mapya.

Kuna askari 2,500 wa Marekani nchini Iraq hivi sasa, na muungano unaoongozwa na Marekani umepelekwa Iraq kusaidia jeshi la nchi hiyo kupambana na kundi la IS kwa kutoa mafunzo na ushauri kwa vikosi vya Iraq.