Wanafunzi wa kilimo Tanzania waomba wataalamu kupima udongo
2021-08-16 07:37:22| cri

Wanafunzi wa Chuo cha Kilimo cha Mbalizi Polytechnic wamewaomba wataalamu kutoka Taasisi ya Utafiti wa Kilimo nchini Tanzania (TARI) Kituo cha Uyole, kupima afya ya udongo ili kuendelea kuzalisha miche ya mazao kwa ubora unaotakiwa na kujiingizia kipato.

Wanafunzi hao wamesema hitaji lao kwa sasa ni kupimiwa afya ya udongo chuoni mwao kwa ajili ya kuzalisha miche ya aina mbalimbali ikiwamo ya matunda na baadaye kuiuza kwa jamii inayowazunguka.

Wameongeza kuwa hadi sasa TARI-Uyole wamewapatia miche na mbegu za aina mbalimbali pamoja na  elimu ya namna ya kuotesha na kuhudumia mimea hiyo.

Kwa upande wake,Mkurugenzi wa TARI, Kituo cha Uyole, Dk. Tulole Bucheyeki, amesema wamebaini tatizo kubwa kwenye afya ya udongo na wameanzisha mradi wa kupima udongo katika mikoa minne ikiwamo Mbeya, Rukwa na Morogoro.

Alisema wataalamu wa kituo hicho watakuwa wanapima udongo ili kujua tatizo lililopo pamoja na kutoa ushauri wa kitaalamu kwa ajili ya kuongeza uzalishaji wa mazao.