Wadhibiti wa nishati Afrika mashariki wairai serikali
2021-08-30 08:05:00| CRI

Jumuia ya Wadhibiti wa Huduma ya Nishati ya Afrika Mashariki wameiomba Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kuunga mkono jitihada za ujenzi wa Taasisi ya Mafunzo ya Udhibti wa Nishati Afrika Mashariki ambayo inatarajiwa kujengwa nchini. Katibu Mtendaji wa Jumuiya ya Wadhibiti wa Huduma za Nishati Afrika Mashariki, Dk. Geoffrey Mabea, alitoa rai hiyo alipozungumza na kujitambulisha kwa Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar ofisini kwake Vuga, Zanzibar.

Alisema jumuiya hiyo imepanga kujenga taasisi itakayotoa mafunzo kwa watu wake kwa lengo la kuwajengea uwezo wa kitaalamu watendaji kutoka nchi wananchama.

Dk. Geoffrey alisema hatua hiyo itasaidia kuitangaza Tanzania na Afrika Mashariki kwa kuwaanda wataalamu wengi ambao watasaidia Afrika na dunia kwa ujumla katika masuala ya huduma za nishati.

Alisema jumuiya hiyo ambayo makao makuu yake yako jijini Arusha, tayari imekwishatayarisha masuala ya msingi kwa ajili ya utekelezaji wa azma hiyo ambapo viongozi wa jumuiya hiyo wanaendelea kutafuta eneo mahususi kwa ajili ya ujenzi wa taasisi hiyo ya mafunzo.