Wataalamu wa Kenya watoa mwito wa kubadili sera ili kuchochea ukuaji unaohimili mabadiliko ya tabianchi
2021-09-03 09:09:54| CRI

Wataalamu wa Kenya wamesema lengo la ukuaji unaohimili mabadiliko ya tabianchi linaweza kutimizwa kwa kurekebisha sera na sheria zilizopo pamoja na kushirikiana zaidi na sekta ya viwanda na jamii.

Wakiongea kwenye awamu ya kwanza ya Shule ya Majira ya Joto kuhusu Haki ya Tabianchi inayoendelea mjini Nairobi, wataalamu wamesisitiza hitaji la sera za maendeleo na uwekezaji kwenye teknolojia safi ili kutia mkazo katika ajenda ya mazingira ya Kenya.

Joseph Kurauka, msomi wa masuala ya mazingira alisema sera wezeshi na mfumo wa usimamizi vinahitajika kufanikisha juhudi za Kenya kuelekea lengo la usawa kati ya utoaji na unyonyaji wa hewa ya ukaa (Carbon neutrality) wakati wa kudumisha ukuaji wa kasi wa uchumi.

Bw. Kurauka amesema kuna haja ya kuingiza ustahimilivu wa mabadiliko ya tabianchi kwenye mipango ya maendeleo ya taifa, ili kupunguza kadri iwezekanavyo athari kwa riziki za watu na maliasili.