Msomi wa Somalia: China yainua kwa kiasi kikubwa imani ya nchi za Afrika ya kujitegemea na kujiamulia mambo
2021-09-07 15:15:51| CRI

Msomi wa Somalia: China yainua kwa kiasi kikubwa imani ya nchi za Afrika ya kujitegemea na kujiamulia mambo_fororder_93715657

Msomi wa Somalia na naibu mtafiti wa Taasisi ya Utafiti wa Afrika katika Chuo kikuu cha ualimu cha Zhejiang Dkt. Hodan Osman Abdi anaona, maendeleo ya China na jinsi inavyozitendea nchi za Afrika kwa usawa, vimeziongezea nchi za Afrika imani ya kujitegemea na kujiamulia mambo.

Akihojiwa hivi karibuni na mwanahabari wa Shirika Kuu la Utangazaji la China CMG, Dkt. Hodan amesema “China na nchi nyingi za Afrika ikiwemo Somalia zilikuwa na historia inayofanana ya kupambana na ubepari na ukoloni. Hivi sasa, wakati nchi nyingi za Afrika bado zinaendelea kutafuta suluhu ya kisiasa ili kutimiza umoja wa taifa na maendeleo endelevu na shirikishi, China imetimiza hilo chini ya uongozi wa Chama cha Kikomunisti cha China.”

Dkt. Hodan ambaye ameishi nchini China kwa miaka 16, ameshuhudia mafanikio makubwa yaliyopatikana China katika kutimiza maendeleo ya taifa. Kabla ya kuja China kujiendeleza kielimu, picha aliyokuwa nayo kuhusu China ilikuwa ni “kuna mashamba kila mahali, kila mtu anajua kungfu”. Baada ya kupata elimu kamili ya juu nchini China katika miaka 16 iliyopita, Dkt. Hodan amepata ufahamu wa kina kuhusu sababu ya mafanikio ya China. Alisema, mamia ya mamilioni ya wachina wameondokana na umaskini uliokithiri tangu China ilipoanza kufanya mageuzi na kufungua mlango. Hivi leo watu wa China wanafurahia maisha kutokana na miundombinu kamili na yenye ufanisi, huduma nzuri za matibabu na elimu yenye ubora. Mwaka 1978, wakati China ilipoanza kutekeleza sera ya mageuzi na ufunguaji mlango, nchi nyingi duniani pia zilikuwa zimeweka mipango kabambe ya maendeleo iliyofanana na ule wa China. Hadi leo mipango hiyo ya baadhi ya nchi bado iko kwenye makaratasi tu, lakini maendeleo ya China yametoka kwenye karatasi na kuwa hali halisi.

Dkt. Hodan anaona sababu ya mafanikio hayo ya China ni kuwa Chama cha Kikomunisti cha China (CPC) kimefanikiwa kuwashikamanisha watu wa China, kuchochea azma na ari yao. Ingawa watu wa China wana sifa kubwa ya uchapaji kazi na ustahimilivu, lakini uvumbuzi uliofanywa na CPC ni kuweza kuhamasisha na kuchochea sifa hiyo kadri inavyowezekana, na kuelekeza nguvu zote kwa lengo moja. Dkt. Hodan alisema, sababu ambayo CPC kimeweza kustawi katika miaka 100 iliyopita, ni kuwa hakijasahau hata siku moja lengo lake la asili la kutumikia maslahi ya wananchi.

Dkt.Hodan alisema utawala bora na utulivu nchini China umeweka mfano wa kuigwa kwa Somalia. Hivi sasa Somalia iko katika kipindi muhimu cha maendeleo ya nchi, wasomi wa nchi hizo mbili kubadilishana maoni na uzoefu kwenye nyanja ya usimamizi wa jamii, kuna maana kubwa kwa Somalia.

Dkt. Hodan anaona kuwa nguvu ya ushawishi ya China kwa nchi za Afrika ikiwemo Somalia inaonekana katika kila nyanja. Akitolea mfano wa vyombo vya habari, alisema vyombo vya habari vya China vilivyoko barani Afrika vimeongeza anuwai na kutia rangi katika mazingira ya vyombo vya habari ya Afrika. Katika muda mrefu uliopita, maoni ya umma barani Afrika yalikuwa yamedhibitiwa na vyombo vya habari vya Magharibi, ambavyo ripoti zao huchochea migogoro na migawanyiko kati ya nchi, na kuangusha imani ya watu kwa serikali zao. Lakini vyombo vya habari vya China ni tofauti kabisa, vinazingatia zaidi kutoa ripoti zinazohusiana na maendeleo kwa mtazamo wa kiujenzi na katika msingi wa kufuata ukweli, na kuwa na athari chanya kwa vyombo vya habari vya Afrika.

Akizungumzia ushirikiano kati ya Somalia na China, Dkt. Hodan alisema ushirikiano kati ya nchi hizo mbili kwenye sekta ya afya una umuhimu wa kihistoria. Tangu janga la Corona lilipoibuka, China imekuwa ni nchi ya kwanza kutoa msaada kwa Somalia, na vifaa tiba na chanjo zilizotolewa na China vimetoa mchango mkubwa katika mapambano ya Somalia dhidi ya janga hilo. Anaamini kuwa urafiki wa dhiki na faraja kati ya nchi hizo mbili hakika utasukuma mbele ushirikiano hadi kufikia kiwango kipya.

Dkt. Hodan anatarajia Baraza la Ushirikiano kati ya China na Afrika (FOCAC) litaunga mkono zaidi maendeleo ya Somalia. Amesema, FOCAC siku zote ni jukwaa muhimu la kuunga mkono maendeleo ya Afrika, na jinsi China inavyozitendea kwa usawa nchi za Afrika katika jukwaa hilo imeziongezea imani ya kujitegemea na kujiamulia mambo. Amesema anatarajia kuwa mkutano ujao wa FOCAC utakaofanyika mwaka huu nchini Senegal, utafungua ukurasa mpya wa ushirikiano kati ya Somalia na China. Dkt. Hodan amesema Somalia ina hali nzuri ya kijiografia, maliasili nyingi na idadi kubwa ya vijana, anatarajia kuwa FOCAC itaunga mkono zaidi miradi inayohitajika zaidi ya maendeleo ya Somalia ikiwemo ujenzi wa miundombinu, na kuisaidia Somalia kubadilisha raslimali ilizonazo kuwa matokeo halisi ya maendeleo.