Vijana wana nafasi muhimu kwenye uhusiano kati ya China na nchi za Afrika
2021-10-20 15:12:52| CRI

Vijana wana nafasi muhimu kwenye uhusiano kati ya China na nchi za Afrika_fororder_222

Tamasha la sita la mawasiliano ya vijana kati ya China na Afrika limefunguliwa jana Jumanne mjini Beijing, likiwakutanisha vijana wa China na wenzao kutoka nchi mbalimbali za Afrika. Tamasha hilo linafanyika chini ya utaratibu wa Baraza la Uhusiano kati ya China na Afrika.

Pamoja na mambo mengine, washiriki wa tamasha hili wanafuatilia miaka 100 ya Chama cha Kikomusti cha China CPC, na mchango wake katika juhudi za maendeleo za China. Akiongea na Idhaa ya Kiswahili ya Radio China Kimataifa baada ya ufunguzi wa mkutano huo, aliyekuwa balozi wa China nchini Tanzania Madam Wang Ke, amesema tamasha hili ni utaratbu mzuri kwa uhusiano kati ya China na nchi za Afrika, hasa ikizingatiwa kuwa vijana ndio mustakbali wa uhusiano kati ya pande hizo mbili.

Madam Wang Ke amesema licha ya kuwa tamasha la safari hii linafanyika wakati wa changamoto ya COVID-19, waandaaji wamefanya maandalizi mazuri kwa ajili ya washiriki kuweza kubadilishana mawazo na kushiriki katika shughuli mbalimbali za mabadilishano ya kiutamaduni. Amesema ni bahati mbaya kuwa changamoto ya COVID-19 imefanya safari hii washiriki kutoka nchi za Afrika wawe ni wale wanaoishi Beijing, na angependa zaidi vijana kutoka Afrika waje China kubadilishana mawazo na wenzao wa China na waione China wao wenyewe, na wakirudi nyumbani wawafahamishe ndugu zao, na hata watu wengine kupitia mitandao ya kijamii, radio, magazeti na televisheni.

Akizungumzia kuhusu kufahamiana na kuelewana kati ya pande mbili, Madam Wang amesema licha ya kuwa uhusiano kati ya China na nchi za Afrika ni mzuri, bado kuna tatizo la kuelewana vibaya. Amesema angependa kuona vijana zaidi wa China wanajifunza kuhusu historia, utamaduni na hata jamii za Afrika ili kuondoa hali ya kuelewana vibaya.