Kupambana na umaskini kwa kulenga kunaweza kuleta maendeleo ya haraka katika nchi za Afrika
2021-10-21 15:43:59| cri

Tamasha la sita la vijana wa China na nchi za Afrika linaendelea kufanyika mjini Beijing, ambapo vijana wa China na wenzao wa Afrika wanabadilishana mawazo kuhusu mambo ya siasa, maendeleo na utamaduni.

 

Kwenye mjadala kuhusu maendeleo, vijana wa China na wenzao wa Afrika wamegusia mambo mengi yanayohusu juhudi za kupambana na umaskini. Imeonekana kuwa umaskini ni changamoto iliyokuwa ikizisumbua China na nchi za Afrika, lakini kutokana na uongozi wa Chama cha Kikomunisti cha China, mwaka 2020 China ilitanganza kuwa imetokomeza umaskini uliokithiri, na sasa watu wake wanaishi katika hali nzuri zaidi ikilinganishwa na ilivyokuwa miongo minne iliyopita. Lakini changamoto hiyo bado inaendelea kuzitatiza nchi za Afrika. Washiriki wengi wameona kuwa nchi za Afrika zina mambo mengi ya kujifunza kutoka China kwenye kupambana na umaskini.

 

Aliyekuwa balozi wa China nchi Tanzania Madam Wang Ke, anajua vizuri changamoto za nchi za Afrika kwenye kupambana na umaskini. Amesema licha ya kuwa baadhi ya nchi za Afrika kama Tanzania zimekuwa na ongezeko la uchumi, hali halisi ni kuwa ongezeko hilo halijaweza kuwanufaisha moja kwa moja watu wa kawaida. Anaona kuwa ni jambo la muhimu kama uwekezaji ukielekezwa zaidi kwenye maeneo yanayoweza kuhimiza zaidi maendeleo. Ametaja kuwa sekta ya elimu ni moja ya maeneo hayo, na anaona litakuwa ni jambo la muhimu zaidi kama kukiwa na uwekezaji kwenye kuandikisha wanafunzi zaidi kutoka maeneo ya vijijini.

 

Eneo ambalo juhudi za kupambana na umaskini zinaonekana wazi zaidi ni vijijini, ambako umaskini uko wazi zaidi tofauti na mijini. Madam Wang anaona kuwa jambo la muhimu ambalo nchi za Afrika zinaweza kujifunza, ni kupambana na umaskini hadi mashinani. Amesema maeneo ya vijijini kwa mfano yakiwa na lengo moja kwenye mkakati wa maendeleo na kusimamia vizuri utekelezaji wa mikakati hiyo, hali ya umaskini inaweza kutoweka haraka.