“Miradi Tisa” yaongeza ubora na ufanisi wa ushirikiano kati ya China na Afrika
2021-12-01 15:09:49| CRI

Kufuatia rais Xi Jinping kutoa hotuba kwa njia ya video kwenye ufunguzi wa Mkutano wa Nane wa Mawaziri wa Baraza la Ushirikiano kati ya China na Afrika (FOCAC), Mkurugenzi wa Taasisi ya Utafiti wa Afrika ya Chuo Kikuu cha Ualimu cha Zhejiang Prof. Liu Hongwu, alipohojiwa na mwanahabari wetu amesema kuanzia “Mipango Kumi ya Ushirikiano” iliyotolewa kwenye Mkutano wa Kilele wa FOCAC uliofanyika Johannesburg, hadi “Hatua Nane” zilizotolewa kwenye Mkutano wa Kilele wa Beijing, hadi “Miradi Tisa” iliyotangazwa na Rais Xi kwenye mkutano wa Dakar, ushirikiano kati ya China na Afrika umeendelea kuinua kiwango chake cha ubora na ufanisi, huku njia ya ushirikiano huo ikizidi kuwa pana.

“Miradi Tisa” yaongeza ubora na ufanisi wa ushirikiano kati ya China na Afrika

Unaochukua nafasi ya kwanza kwenye Miradi Tisa ni Mradi wa Huduma za Afya. Wakati kirusi kipya kilichobadilika cha Corona aina ya Omicron kimetoa changamoto mpya kwa juhudi za dunia kupambana na janga la COVID-19, ahadi ya China ya kutoa dozi nyingine bilioni moja za chanjo dhidi ya virusi vya Corona, imeonyesha mara nyingine dhamira ya China ya kushikamana na Afrika kwenye mapambano dhidi ya janga hilo. Profesa Liu Hongwu anaona Afrika ikiwa ni eneo dhaifu kwenye mapambano hayo ya kimataifa, uungaji mkono wa China kwa Afrika kwenye mapambano hayo kamwe si maneno matupu, bali siku zote umetekelezwa kwa vitendo halisi.

“Nchi za Afrika kwa ujumla zina watu bilioni 1.3, kwa hiyo dozi bilioni moja zitatosha kwa makundi yote ya watu walio hatarini zaidi kuambukiziwa katika nchi zote zilizoathirika zaidi na janga la Corona. Dozi hizi bilioni moja zinawakilisha uungaji mkono thabiti wa China kwa nchi za Afrika kwenye mapambano dhidi ya janga hili, ahadi ya China kamwe si maneno matupu, bali siku zote imetekelezwa kivitendo. Ili kuhakikisha dozi hizi za chanjo zinaweza kuwafikia watu wenye mahitaji, China pia imeweka hatua za ziada, kwa mfano kutekeleza miradi kumi ya ushirikiano kwenye sekta ya afya na matibabu, kutuma wataalamu wa afya na wahudumu wa matibabu 1,500 kwenye nchi za Afrika katika miaka mitatu ijayo. Hatua hizo zitatoa mchango mkubwa kwa nchi za Afrika kupambana na janga la virusi vya Corona.”Amesema profesa Liu.

Profesa Liu Hongwu anaona “Miradi Tisa” inaonesha kuwa ushirikiano wa China na Afrika umekuwa ukitilia maanani zaidi kukidhi mahitaji ya nchi za Afrika, na kuboresha maisha ya watu wa huko. Mradi mkubwa wa pili katika Mirada Tisa ni kupunguza umaskini na kuendeleza kilimo, ambao utatekeleza miradi kumi ya kupunguza umaskini na kukuza kilimo barani Afrika, kutuma wataalamu 500 wa kilimo kwenye nchi za Afrika, na kujenga vituo vya mawasiliano na mafunzo ya teknolojia za kilimo kati ya China na Afrika nchini China. Profesa Liu amesema, “Mradi wa Kupunguza Umaskini na Kuendeleza Kilimo” unalenga kuwanufaisha kihalisi wakulima wa Afrika kutokana na matunda ya ushirikiano kati ya China na Afrika, ili kuzisaidia nchi za Afrika kuimarisha msingi wa maendeleo ya uchumi na jamii. Amesema,

“Mipango hii ya China ya kuendeleza ushirikiano na Afrika, inazingatia zaidi kuboresha maisha ya watu wa Afrika, na kusukuma mbele juhudi za kupunguza umaskini katika nchi za Afrika, ili kuwanufaisha kihalisi waafrika. Afrika ni bara ambalo kilimo ni uti wake wa mgongo, na asilimia kubwa ya watu wanategemea kilimo kujipatia riziki zao. Zamani wakulima wa Afrika walikuwa ni kundi la watu maskini zaidi. Lakini sasa Miradi Tisa inalenga kuwanufaisha wakulima wa Afrika, hatua inayoonesha dhana mpya ya ushirikiano kati ya China na Afrika inayotoa kipaumbele kwa watu.”

Profesa Liu Hongwu amesema “Miradi Tisa” si kama tu itasaidia kuimarisha msingi wa maendeleo ya Afrika, bali pia inatupia macho kujenga mustakbali wa siku za baadaye. Kwenye Mradi wa Mavumbuzi ya Kidijitali ambao pia ni moja ya Miradi Tisa, China itaisaidia Afrika kutekeleza miradi kumi ya uchumi wa dijitali, kujenga kituo cha ushirikiano wa satelaiti kati ya China na Afrika, kuunga mkono ujenzi wa maabara ya pamoja kati ya China na Afrika, taasisi za pamoja za utafiti na vituo vya ushirikiano kwenye mavumbuzi ya sayansi na teknolojia na kadhalika. Profesa Liu Hongwu amesema, Afrika yenye idadi kubwa ya vijana, ina mustakbali mkubwa wa kukuza uchumi wa dijitali. Katika miaka ya hivi karibuni, ushirikiano wa uchumi wa dijitali kati ya China na Afrika umekua kwa kasi, ambapo kampuni za China zimeshiriki kwenye miradi mbalimbali ya kutandaza mkonga wa chini ya bahari unaoiunganisha Afrika na mabara ya Ulaya, Asia na Amerika; kutimiza lengo la huduma za mawasiliano ya simu kupatikana katika bara zima kwa kushirikiana na mashirika makubwa ya huduma za mawasiliano ya Afrika, kujenga zaidi ya nusu ya vituo vya mtandao wa internet na mtandao wa internet wa kasi barani Afrika, na kutandaza mkonga wenye urefu wa kilomita zaidi ya laki mbili, ambao umesaidia familia milioni 6 kuunganishwa kwenye mtandao wa kasi na kutoa huduma kwa jumla ya watu milioni 900 wa Afrika. Mradi wa Mavumbuzi ya Dijitali utazidi kuzisaidia nchi za Afrika kuziba “pengo la dijitali”, ili kutandika njia mpya ya ushirikiano wa China na Afrika katika siku zijazo. Amesema, 

“Ushirikiano kati ya China na Afrika sasa unazingatia zaidi mwelekeo mpya wa maendeleo unaotupia macho siku za baadaye, yaani kusukuma mbele kwa kiwango cha juu ujenzi wa Jumuiya yenye hatma ya pamoja kati ya China na Afrika kwenye mwanzo huu mpya na katika zama mpya. Unazihitaji China na Afrika zisukume mbele ushirikiano wenye uratibu wa hali ya juu kwenye uchumi wa dijitali, elimu ya kidijitali, usimamizi wa dijitali na upunguzaji wa umaskini kwa njia ya dijitali. Katika mradi huu, tutatumia njia mpya ya kisasa na ya kivumbuzi kuziba pengo la kidijitali linaloyakabili maendeleo ya Afrika, na vilevile kutumia fursa ya kuwepo vijana wengi barani Afrika. Naona hali hii inaonesha mwendelezo na uratibu kati ya Miradi Tisa ya ushirikiano, ambayo si kama tu inatilia maanani kuimarisha msingi, na bali pia inazingatia kujenga mustakbali wa siku za baadaye, naamini itatoa fursa mpya kwa maendeleo ya Afrika katika mwongo mmoja au miongo miwili ijayo.”

Profesa Liu Hongwu anaona, tangu Baraza la Ushirikiano kati ya China na Afrika (FOCAC) lilipoanzishwa hadi leo, ushirikiano kati ya pande hizo mbili umekuwa ukiendelea kuinuka kila baada ya miaka mitatu. Ushirikiano huo si kama tu una mwendelezo wa kihistoria, na bali pia unaendana na wakati na kukumbatia mavumbuzi. Anaona, “Miradi Tisa” imedhihirisha mara nyingine tena kuwa katika kila kipindi muhimu cha maendeleo ya ushirikiano huo, China na Afrika zote zimekuwa zikitupia macho siku zijazo, kuendelea kutafuta fursa mpya na njia mpya za ushirikiano kati ya pande hizo mbili, na kusukuma mbele uhusiano kati ya China na Afrika uendelee kupiga hatua mbele.