Gazeti la New York Times lafichua uhalifu wa kivita wa jeshi la Marekani katika nchi za nje
2021-12-23 15:22:56| CRI

Gazeti la New York Times lafichua uhalifu wa kivita wa jeshi la Marekani katika nchi za nje_fororder_VCG31N679635

Gazeti la New York Times la Marekani hivi karibuni limetoa ripoti, likifichua kwamba, katika miaka ya hivi karibuni, operesheni za kijeshi za nchi hiyo katika Mashariki ya Kati zimesababisha idadi kubwa ya vifo vya raia wasio na hatia. Serikali ya Marekani imekuwa ikipuuza hasara za raia zinazosababishwa na operesheni zake za kijeshi, na kuchukua njia zote kuzuia jumuiya ya kimataifa kufanya uchunguzi. Hata hivyo, mauaji ya raia wasio na hatia hauwezi kusamehewa, na uhalifu wa kivita wa jeshi wa Marekani lazima uchunguzwe.

Gazeti hilo limenukuu zaidi ya nyaraka 1,300 za siri kutoka Wizara ya Ulinzi ya Marekani, zikionesha kwamba mashambulizi mengi ya angani yaliyofanywa na jeshi la Marekani katika nchi za Mashariki ya Kati yalitiwa alama kuwa “makosa makubwa ya kijasusi”, na yalisababisha vifo vya maelfu ya raia, wakiwemo wanawake na watoto wengi. Nyaraka hizo zinaonyesha kuwa tangu mwaka 2014 hadi mwaka 2019, Marekani ilianzisha mashambulizi zaidi ya 50,000 ya angani katika nchi mbalimbali zikiwemo Iraq, Syria na Afghanistan, bila ya kutunga mipango mizuri. Kutokana na kazi ya uzembe ya kijasusi na vitendo vya haraka, jeshi la Marekani halikuweza kuhakikisha watu walioshambuliwa ni magaidi au raia.

Mara kwa mara serikali ya Marekani imekuwa ikidai kwamba kwa sababu ya matumizi ya ndege zisizo na rubani na silaha zinazoongozwa kwa usahihi mkubwa, jeshi la Marekani linaweza kuepuka majeruhi ya raia wasio na hatia katika mashambulizi ya anga. Hata hivyo, kwa mujibu wa takwimu zilizotolewa na jeshi la Marekani lenyewe, wakati wa vita dhidi ya magaidi nchini Iraq na Syria, raia 1,417 wa kawaida waliuawa katika mashambulizi ya angani yaliyofanywa na jeshi la Marekani, na tangu mwaka 2018, mashambulizi ya angani ya Marekani yamesababisha vifo vya raia 188 nchini Afghanistan. Lakini kutokana na takwimu za jumuiya ya kimataifa, idadi halisi ya vifo vya raia katika mshambulizi ya jeshi la Marekani ni zaidi ya mara 10.

Tukio jipya la vifo vya raia nchini Afghanistan kutokana na mashambulizi ya Marekani lilitokea Agosti 29 mwaka huu. Wakati huo jeshi la Marekani lilianzisha mashambulizi ya ndege zisizo na rubani baada ya kundi la Taliban la Afghanistan kuteka mji wa Kabul. Hapo awali Wizara ya Ulinzi ya Marekani ilidai kuwa shambulio hilo lilifanikiwa kuwaua magaidi wengi, lakini baadaye kutokana na ripoti za vyombo vya habari, Marekani ilikiri kuwa shambulio hilo halikuwapata magaidi, badala yake lilisababisha vifo vya raia 10 wakiwemo watoto 7.

Hivi karibuni Marekani ilitoa matokeo ya uchunguzi huo, na kutangaza kuwa hakuna Mmarekani yeyote anayestahili adhabu kutokana na tukio hilo, kwani hakuna uzembe, makosa au uongozi mbaya.

Marekani pia inazuia jumuiya ya kimataifa kuchunguza uhalifu wake wa kivita. Mnamo Machi 2020, Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu ilitangaza uchunguzi kuhusu uhalifu wa kivita na kibinadamu uliofanywa na jeshi la Marekani nchini Afghanistan. Mnamo Septemba mwaka huo, Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani ilitangaza kuweka vikwazo vya upande mmoja kwa Fatou Bensouda, ambaye ni mwendesha mashtaka wa Mahakama hiyo, pamoja na maafisa wengine kadhaa wakuu.

Kwa muda mrefu, Marekani imeanzisha vita nyingi dhidi ya nchi nyingine kwa kisingizio cha demokrasia na haki za binadamu. Lakini vita hizo zimesababisha idadi kubwa ya vifo vya raia. Marekani inapaswa kujibu kwa dhati wito wa jumuiya ya kimataifa, na kuchunguza kwa dhati vitendo vya majeshi yake vya uhalifu wa kivita, ili kuwapoza watu waliouzwa bila ya hatia.