Tanzania yaimarisha hatua za kujikinga na COVID-19
2021-12-27 10:12:13| CRI

Mamlaka za afya za Tanzania bara na Zanzibar zimeimarisha hatua za kujikinga na COVID-19 haswa kwa wale wanaosafiri kimataifa.

Taarifa ya pamoja iliyotolewa na Wizara za afya za Tanzania bara na Zanzibar imesema mamlaka zote katika forodha zinatakiwa kuhakikisha wasafiri na wafanyakazi wanafuata hatua za kinga na udhibiti zikiwemo kutumia vitakasa mikono, umbali wa kijamii na kuvaa barakoa.

Taarifa pia imesema kujaza Fomu ya Ufuatiliaji wa Hali ya Afya ya Wasafiri ni matakwa ya lazima kabla ya kwenda Tanzania na adhabu zitatolewa kwa wale wanaokiuka kanuni.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, wasafiri wote wakiwemo Watanzania na wakazi wanaorudi wanatakiwa kuonesha vyeti vyenye matokeo hasi ya kipimo cha virusi vya Corona wakati wanapowasili.